Sunday, October 26, 2025

RAIS DKT. SAMIA AKUTANA NA UJUMBE WA JUKWAA LA MABUNGE LA NCHI ZA MAZIWA MAKUU (FP-ICGLR) IKULU NDOGO TUNGUU, ZANZIBAR



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Kiongozi wa Jukwaa la Mabunge la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR) Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Domitien Ndayizeye Ikulu ndogo Tunguu, Zanzibar, tarehe 26 Oktoba, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa Jukwaa la Mabunge la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR) ukiongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Domitien Ndayizeye, Ikulu ndogo Tunguu, Zanzibar, tarehe 26 Oktoba, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na ujumbe wa Jukwaa la Mabunge la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR) ukiongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Domitien Ndayizeye, Ikulu ndogo Tunguu, Zanzibar, tarehe 26 Oktoba, 2025. FP-ICGLR ni miongoni mwa misheni mbalimbali zilizowasili nchini kwa ajili ya uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Kiongozi wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Uganda, Dkt. Speciosa Wandira Kazibwe mara baada ya mazungumzo, Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar, tarehe 26 Oktoba, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Ujumbe wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulioongozwa na Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Uganda, Dkt. Speciosa Wandira Kazibwe Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar, tarehe 26 Oktoba, 2025.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akionesha Tuzo ya Presidential Global Water Changemakers 2025 ambayo alitunukiwa tarehe 13 Agosti, 2025 Cape Town, nchini Afrika Kusini. Tuzo hiyo iliwasilishwa kwake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Ikulu Tunguu Zanzibar tarehe 26 Oktoba, 2025. Tuzo hiyo ya Ulimwengu ya Marais wanaoleta Mabadiliko katika Sekta ya Maji imetolewa kwa kutambua uongozi bora na dhamira ya dhati katika kuanzisha na kuendeleza mipango na miradi ya Maendeleo katika Sekta ya maji nchini Tanzania.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 26 Oktoba 2025, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Jukwaa la Mabunge la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR), ukiongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Burundi, Mheshimiwa Domitien Ndayizeye, katika Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar.

Mazungumzo hayo yalijikita katika masuala ya demokrasia, amani na ushirikiano wa kikanda, huku ujumbe huo ukiwa miongoni mwa misheni mbalimbali ya kimataifa iliyowasili nchini kwa ajili ya uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.

Rais Dkt. Samia aliukaribisha ujumbe huo kwa ukarimu na kueleza kuwa Tanzania imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora. Aidha, alisisitiza kuwa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha hali ya usalama inabaki kuwa shwari katika kipindi chote cha uchaguzi.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Domitien Ndayizeye alitoa pongezi kwa Tanzania kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi na kwa kuendeleza utamaduni wa kisiasa wa amani na umoja unaoitambulisha nchi hiyo katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Ameeleza kuwa FP-ICGLR, kama taasisi ya kikanda inayojikita katika kukuza demokrasia na utawala bora, itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha michakato ya kisiasa inatekelezwa kwa misingi ya haki, ushirikishwaji na utulivu.

Mazungumzo hayo yanaendelea kuonyesha dhamira ya Tanzania katika kushirikiana na jumuiya za kikanda na kimataifa katika kulinda amani, demokrasia na maendeleo endelevu barani Afrika.

#RaisSamia #FPICGLR #Uchaguzi2025 #TanzaniaInajengaDemokrasia #AmaniNaUmoja #Zanzibar

 

RAIS DKT. MWINYI AKUTANA NA MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA UMOJA WA AFRIKA
















Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo amefanya mazungumzo na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AUEOM), ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Botswana, Mheshimiwa Mokgweetsi Masisi, Ikulu Zanzibar. Mheshimiwa Masisi aliambatana na ujumbe wa maafisa waandamizi kutoka AUEOM walioko nchini kwa ajili ya kufuatilia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi aliwakaribisha wageni hao na kuwapongeza kwa hatua ya Umoja wa Afrika kutuma timu ya waangalizi kama sehemu ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, amani na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia barani Afrika.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha mazingira yote ya uchaguzi yanabaki kuwa salama na yenye amani, akisisitiza kuwa Zanzibar imejipanga vyema kwa zoezi hilo muhimu la kidemokrasia. “Hali ya ulinzi na usalama ni shwari, na wananchi wako tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi,” alisema Rais Mwinyi.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha taratibu zote za uchaguzi zinafuatwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wao, ujumbe wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AUEOM) umepongeza hatua za maandalizi zilizochukuliwa na Serikali ya Zanzibar, hususan katika kuhakikisha mjumuisho wa makundi maalum ya jamii kama vile wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mchakato wa uchaguzi.

Viongozi hao wamesema kuwa Umoja wa Afrika unaendelea kufuatilia mwenendo wa maandalizi ya uchaguzi nchini Tanzania kwa lengo la kuhakikisha chaguzi zinazoendeshwa barani Afrika zinakuwa huru, haki na zenye uwazi. Wameongeza kuwa ni matarajio yao kuwa uchaguzi wa mwaka huu, Tanzania Bara na Zanzibar, utaendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine katika kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Mheshimiwa Masisi aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ukarimu na ushirikiano walioupata tangu walipowasili, akisisitiza kuwa ujumbe wake una imani kubwa na dhamira ya Tanzania ya kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na kufanyika kwa misingi ya sheria na taratibu zote husika.

Mazungumzo hayo ni sehemu ya ratiba ya mikutano ya Misheni hiyo ya AUEOM na viongozi mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ufuatiliaji wa mchakato mzima wa uchaguzi wa mwaka 2025

WASIMAMIZI WA VITUO VYA KUPIGIA KURA WATAKIWA KUTOA KIPAUMBELE KWA WAPIGA KURA WENYE MAHITAJI MAALUMU SIKU YA UCHAGUZI MKUU












Wasimamizi wa Vituo vya Kupigia Kura  Jimbo la Kilombero wametakiwa kuhakikisha wanatoa Kipaumbele kwa wapiga kura wenye Mahitaji Maalumu pindi watakapofika Kituoni siku ya Uchaguzi Mkuu Tarehe 29 Oktoba 2025.

Rai hiyo Imetolewa Leo tarehe 26 Oktoba 2025 na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kilombero Bi. Joha Mlindwa wakati akifungua Mafunzo ya Siku Mbili  kwa Wasimamizi wa Vituo vya Kupigia Kura yanayofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba uliopo Ifakara.

" Ninyi  ndio watendaji mnaokutana na wapiga kura, hivyo hakikisheni mnazingatia unadhifu, lugha nzuri na kutoa Kipaumbele kwa wapiga kura wenye Mahitaji Maalumu pindi watakapofika Kituoni kama Wajawazito, Watu wenye ulemavu, Wazee n.k ". Alisema Bi. Joha Mlindwa

Aidha Bi. Joha Mlindwa aliwasisitiza Wasimamizi  katika Vituo kuhakikisha Wanazingatia  kwa Umakini Katiba, Sheria, Kanuni ,Miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi .

"Tangu siku ya Uteuzi wenu Ninyi ni Watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,  mtawajibika kwa Tume na sio kwa mamlaka nyingine katika Utekelezaji wa Majukumu yenu ya Uchaguzi hivyo mzingatie Mafunzo mtakayopewa". Alieleza Bi. Joha

Aidha Wasimamizi hao walikula Kiapo cha Kutunza Siri na Tamko la Kujitoa uanachama wa Chama cha Siasa au kutoka Mwanachama wa Chama cha Siasa mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kilombero Bi. Joha Mlindwa.

Mmoja wa Wasimamizi hao wa Vituo vya Kupigia Kura wanaopatiwa Mafunzo Bi. Yasinta Victor alisema kuwa wanazingatia Viapo walivyokula na maelekezo yote watakayopewa na Tume ili kufanikisha Uchaguzi Mkuu  Tarehe 29 Oktoba 2025.

Mafunzo hayo yanajumuisha Wasimamizi wa Vituo 597 na Wasimamizi Wasaidizi  1194 katika Vituo 597 Vilivyopo Kata 19 za Halmashauri ya Mji Ifakara.

Friday, October 24, 2025

Waziri Kombo akutana na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika

 
















 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekutana na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AU), na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Botswana, Mhe. Mokqweets Masisi katika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam.

Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya AU iko nchini  kuangalia zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Octoba, 2025, ili kuhakiki Utekelezaji wa Demokrasia ya kweli kupitia Uchaguzi huo, kwa kuzingatia misingi ya haki, uwazi na uhuru. 

Akizungumza katika katika Mkutano huo, Mhe. Kombo amesema Serikali ya Tanzania imefanya jitihada mbalimbali ili  kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na uwazi na unakuwa huru na wa haki.

Mhe. Kombo aliikaribisha kwa dhati Misheni hiyo ya AU nchini na kuipongeza kwa utekelezaji na kufuatilia  zoezi la Uchaguzi Mkuu nchini.

 "Utekelezaji wa misheni kama hii ni changamoto kubwa inayohitaji rasilimali nyingi na jitihada za dhati, na uwepo wa Mheshimiwa Masisi ni ishara ya mshikamano wa kikanda na kujitolea katika demokrasia" Alifafanua Mhe. Balozi Kombo.

Waziri Kombo alielezea mafanikio ya awamu ya kwanza ya tathmini ya awali ya uchaguzi, iliyofanyika Juni 2025, iliyoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Dkt. Pumzille Mlambo–Ngcuka ambapo maoni yaliyotolewa katika tathmini hiyo, yaliimarisha jitihada za Tanzania katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu.

Aidha, Waziri Kombo alieleza azma ya Serikali ya kuimarisha demokrasia katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuahidi ushirikiano kamili wa Serikali na wadau wote wa uchaguzi katika mipango yote ya uchaguzi.

Waziri Kombo pia alisema  takwimu zinaonyesha ongezeko la asilimia 26.5 katika idadi ya wapiga kura, na kuelezea mipango ya kampeni za uchaguzi, elimu kwa wapiga kura, na jitihada za kuelimisha wananchi kupitia mashirika ya kiraia.

"Jitihada hizi zote zinalenga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa usahihi, haki, na kuakisi mapenzi ya wananchi wote wa Tanzania" Alibainisha Mhe. Kombo.

Waziri Kombo pia aliishukuru Misheni hiyo ya AU kwa juhudi zake za kukuza demokrasia na utawala bora, na kuwatakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Naye Mkuu wa Misheni hiyo ya AU Mhe. Masisi aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiamini Misheni hiyo na aliweka bayana kuwa timu yake itazingatia maadili ya Uchaguzi Mkuu pamoja na Sheria na miongozi ya nchi na ya AU katika kutekeleza majukumu yao.

RAIS DKT. SAMIA AKUTANA NA UJUMBE WA JUKWAA LA MABUNGE LA NCHI ZA MAZIWA MAKUU (FP-ICGLR) IKULU NDOGO TUNGUU, ZANZIBAR

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Kiongozi wa Jukwaa la Mabunge la...