Thursday, February 14, 2013

Bunge kutoonyeshwa Live

Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Thomas Kashilila akitoa somo kwa waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa wabunge kuzisoma na kuzitumia ipasavyo  kanuni za bunge ili kuondoa manug'uniko yanayojitokeza pindi wanapozuiliwa na spika kuchangia mijadala au kutoa hoja bungeni kwa sababu ya kukiuka kanuni na umuhimu wa waandishi wa habari  kuzitumia taarifa rasmi za bunge katika utoaji wa taarifa zao.

Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Thomas Kashilila akitoa ufafanuzi kwa  waandishi wa habari kuhusu ukiukwaji wa kanuni za bunge uliofanywa na baadhi ya wabunge wakati wa mkutano wa 10 wa bunge uliomalizika mjini Dodoma na mabadiliko yaliyofanyika kwa baadhi ya kamati kuondolewa  pamoja na uundwaji wa kamati mpya 3 zitakazoshughulikia Ushirikiano wa Afrika, Mashariki, Bajeti na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.Picha na Aaron Msigwa-MAELEZO.

   *********************************************

SIKU chache baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, kulalamikiwa kwa kuendesha Bunge kinyume cha kanuni, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, amewatetea huku akiwatwisha lawama hizo baadhi ya wabunge.
Kutokana na kadhia hiyo ya kukosolewa, Dk. Kashililah alisema kuwa Bunge linaandaa utaratibu wa kusitisha vikao vya Bunge kurushwa moja kwa moja (live) ili kuzuia purukushani za wabunge kuonekana kwa wananchi.
Akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge jana kuhusu shughuli zilizotekelezwa katika Mkutano wa Kumi wa Bunge na mapendekezo ya kuundwa kwa kamati mpya, Dk. Kashililah alisema vurugu zilizojitokeza zilitokana na kutofuatwa kwa kanuni ambazo zipo wazi.
Alisema vurugu zinazotokea ni kutokana na baadhi ya wabunge kutozifahamu vema kanuni au kufanya makusudi, hasa kanuni ya 60 na 68, ambazo kama zingefuatwa hayo yote yasingetokea.
Dk. Kashililah alisema baadhi ya wabunge walikuwa wakishindwa kufuata kanuni kwa makusudi kwa kutumia kifungu kimoja tu cha 68 cha kuomba taarifa, utaratibu au mwongozo bila ya kufuata taratibu zinavyotakiwa badala ya kuombea kanuni iliyovunjwa kwanza ndipo aseme yake.
“Mfano, mbunge anajua kuwa anatakiwa kutumia kanuni ya 68 kuomba taarifa, utaratibu au mwongozo, atasimama, baada ya kusimama ataambiwa na Spika aseme, naye atasema amesimama kwa kanuni ipi na anachoombea taarifa ni nini. Lakini baadhi yao wakiomba tu utaona kabla ya kuruhusiwa hapohapo wanaanza kuzungumza,” alisema.
Aliongeza kuwa hali hiyo ya kuzijua kanuni na kutozifuata ndiyo inasababisha kuwapo kwa vurugu hizo ambazo wakati mwingine kwa kutumia kanuni hizo hizo zinamtaka Spika ama aliyekalia kiti chake kuahirisha Bunge.
Dk. Kashililah alisema wanaamua kutoonesha vikao vya Bunge moja kwa moja kutokana na baadhi ya wabunge kukiuka kanuni, kwa kuzungumza mambo yasiyofaa ili waonwe na wapiga kura wao.
“Bunge ni sehemu ya siasa, na mule ndani zimo pande mbili zinazovutana na kwa wale wabunge waopenda kamera ya televisheni utawaona wanazungumza mambo yasiyofaa hadi mishipa inawasisima ili waonwe na wapiga kura wao, mkitoka na kuwauliza watakwambia ni siasa ile.
“Kina mama ambao wanajua kuwa siku hiyo watauliza maswali utawaona siku hiyo wanavalia kikweli kweli ili waonekane…kwa kweli sisi tunaokaa tunaona mambo mengi na mengine yanasikitisha,” alisema.
Alisema walipoomba kuzima, baadhi yao walitoa onyo kwamba waache, ila Bunge linajipanga kufanya utaratibu wa kukaa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuliwezesha Shirika la Utangazaji la Taifa na televisheni nyingine namna ya kurusha shughuli za Bunge.
“Tunataka kukaa na TCRA, TBC na televisheni nyingine pamoja na waandishi wa magazeti kuangalia namna ya kuweka maadili ya kazi, kwa sababu hata TBC wakati mwingine hawafuati maadili, wanampiga picha Spika Makinda akiwa ameinama huku ikionekana amelala,” alisema. SOURCE: Tanzania Daima

No comments: