Friday, October 25, 2013

Serikali ya Tanzania imeingia mikataba saba na makampuni sita ya Kichina yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7 (Sh. trilioni 2.72) ambazo zitawekezwa kwenye ujenzi wa miradi ya umeme na nyumba za makazi na biashara


 Waziri   Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda  akifungua mkutano wa Biashara kati ya Tanzani na China kwenye Hoteli ya  Dong Fang mjini Guangzhou akiwa katika ziara ya kikazi nhcini China Oktoba 24,2013
 Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji nchini, Juliet Kairuki  akizungumza katika   mkutano wa Biashara kati ya Tanzani ana China kwenye Hoteli ya  Dong Fang mjini Guangzhou. Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri Mkuu,Mizengo Pinda  akiwa katika ziara ya kikazi nhcini China Oktoba 24,2013.
 Baadhi ya washirki wa  mkutano wa Biashara kati ya Tanzania na China  wakimsikiliza Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda wakati  alipofungua mkutano huo kwenye Hoteli ya  Dong Fang mjini Guangzhou akiwa katika ziara ya kikazi nhcini China Oktoba 24,2013.
 Waziri  Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda akipokea  mfano wa ndege kutoka kwa   Mwenyekiti wa Shirika la Ndege la China la Hainan Airlines  ,BW. Chen Feng     baada ya  mazungumzo yao kwenye Hoteli ya  Dong Fang mjini Guangzhou akiwa katika ziara ya kikazi nhcini China Oktoba 24,2013.
 Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda akizungumza na  Mwenyekiti wa Shirika la Ndege la China la Hainan Airlines  ,BW. Chen Feng   kwenye Hoteli ya  Dong Fang mjini Guangzhou akiwa katika ziara ya kikazi nhcini China Oktoba 24,2013.Picha Zote na Ofisi ya Waziri Mkuu
---
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
SERIKALI ya Tanzania leo imeingia mikataba saba na makampuni sita ya Kichina yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7 (Sh. trilioni 2.72) ambazo zitawekezwa kwenye ujenzi wa miradi ya umeme na nyumba za makazi na biashara
 
Makubaliano ya uwekezaji huo mkubwa yameshuhudiwa leo (Alhamisi, Oktoba 24, 2013)  na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mawaziri wengine wa Serikali baada ya kusainiwa kwa mikataba saba ya uwekezaji katika sekta hizo muhimu kwa uchumi wa nchi.

Utiaji saini huo ulifanywa mara baada ya Waziri Mkuu kufungua Kongamano la Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na China (Tanzania China Business Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya Dong Fang, jijini Guangzhou jimboni Guangdong, China. Kongamano hilo ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Baraza la Biashara la China Afrika (China Africa Business Council-CABC) linashirikisha wafanyabiashara wa China na Tanzania.

Mikataba iliyosainiwa leo ni kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na Kampuni ya Tabiau Electric Apparatus Stock Co Ltd (TBEA) ambao ni kwa ajili ya ujenzi wa njia ya umeme ya msongo mkubwa wa 400kV katika Gridi ya Taifa inayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kaskazini Mashariki hadi Arusha.

Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Bw. Felchesmi Mramba ndiye aliyesaini mkataba huo wenye thamani ya dola za marekani milioni 692.7. Bw. Mramba pia alisaini mkataba mwingine na kampuni ya Shanghai Electric Power ambayo ndio itajenga mtambo wa Kinyerezi III.

Mkataba mwingine uliotiwa saini na Mramba ni kati ya Tanesco na kampuni ya China Gezhouba Group Corporation (CGGC) ambao wamekubali kuendeleza mradi wa umeme unaotokana na nguvu ya maji wa Rumakali ambao uko katika mikoa ya nyanda za juu kusini. Miradi hiyo miwili bado iko kwenye ngazi ya upembuzi yakinifu hivyo gharama zake bado hazijajulikana.

Kampuni ya Mkonge Energy Systems Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Tanzania, Bw. Salum Shamte  ilitiliana saini mkataba na kampuni ya Sino Hyro Resources Ltd kwa ajili ya kuendeleza umeme wa nguvu za maji wa Masigira. Mradi huo unagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 136.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Nehemia Mchechu aliweka saini mkataba baina ya NHC na kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE) kwa ajili ya kuliwezesha kifedha shirika hilo liweze kujenga nyumba mbalimbali za makazi na biashara nchini. Mradi huo una thamani ya dola za Marekani milioni 500.

Bw. Mchechu pia aliwekeana saini mkataba mwingine na kampuni ya Poly Technologies  (POLY) wa kuwa na uhusiano kifedha na kiufundi kati ya kampuni hizo ya kichina na NHC kwa ajili ya kujenga nyumba za makazi na biashara  huko Masaki  wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Gharama za mradi huo ni dola za Marekani milioni 200.

Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo (NDC) Bw. Gideon Nassari kwa niaba ya shirika lake aliingia mkataba na kampuni ya China ya Dalian International Economic & Technical Gooperation Group (CDIG) na Kampuni ya Hydro China Kunming Engineering Corporation kwa ajili ya kujenga kituo cha utafiti na mafunzo ya nishati mbadala. Mradi huo una thamani ya dola za Marekani milioni 136.

Mramba na Mchechu kwa nyakati tofauti walisema kwamba utekelezaji wa miradi hiyo utaanza wakati wowote kwani mambo mengi walishayakamilisha kwenye mazungumzo.

Wakati utambulisho, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bibi Julieth Kairuki alisema jumla ya Makampuni na Taasisi 46 zinazowekeza na kufanya biashara Tanzania zinashiriki katika Kongamano hilo ambapo  kwa upande wa China, CABC wameandikisha makampuni 44 yatakayoshiriki kwenye kongamano. Katika Kongamano hilo, TIC imewasilisha mada ya mazingira ya uwekezaji Tanzania na Bodi ya Utalii na Shirika la nyumba la Taifa wamewasilisha mada zinazohusu uwekezaji kwenye sekta ya Nyumba na fursa za utalii nchini Tanzania

Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya nane ya ziara yake ya kikazi kwa mwaliko wa Serikali ya China bado anaendelea na mikutano mbalimbali na leo usiku atazungumza na Watanzania waishio Guangzhou. 

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 24, 2013

No comments: